MKUU WA NDAKI YA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO (COICT ) AKUTANA NA WATUMISHI KUJADILI MAFANIKIO, CHANGAMOTO NA MWELEKEO WA NDAKI
By Norbert O. Kapinga

MKUU WA NDAKI YA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO (COICT ) AKUTANA NA WATUMISHI KUJADILI MAFANIKIO, CHANGAMOTO NA MWELEKEO WA NDAKI

Posted on July 04, 2026

Mkuu wa Ndaki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (CoICT) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Baraka J. Maiseli, ameongoza kikao cha pamoja na watumishi wote wa Ndaki kilicholenga kutathmini utekelezaji wa shughuli za kipindi cha Aprili hadi Juni 2026, kupitia mafanikio yaliyopatikana, kujadili changamoto zinazoikabili Ndaki, pamoja na kuweka mikakati ya utekelezaji wa vipaumbele vya mwaka wa fedha 2026/2027.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Prof. Baraka J. Maiseli alieleza kuwa "CoICT inaendelea kutekeleza kwa vitendo Dira ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM Vision 2061) kwa kuimarisha ubora katika ufundishaji na ujifunzaji, utafiti, ubunifu, ushauri wa kitaalamu, pamoja na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi na wanafunzi".

Katika taarifa yake, Mkuu wa Ndaki aliwasilisha mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi hicho, yakiwemo kuandaliwa na kuhuishwa kwa mitaala ya programu za shahada na uzamili, kupitishwa kwa programu mbalimbali na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), pamoja na kuendelea kuimarika kwa utoaji wa Programu za Maendeleo ya Kitaaluma (Professional Development Programmes – PDPs), ambazo zimechangia kuongeza mapato ya Ndaki.

Aidha, kikao kilipokea taarifa kuhusu mafanikio katika eneo la utafiti na ubunifu, ikiwa ni pamoja na kuandaliwa kwa Kongamano la Utafiti Elimu Tanzania, kuanzishwa kwa mipango ya vituo vya umahiri (Research Centres of Excellence), kupandishwa vyeo kwa baadhi ya watumishi wa kitaaluma, na kuendelea kuimarisha uwezo wa watafiti kupitia programu mbalimbali za maendeleo ya kitaaluma.

Kwa upande wa miundombinu, Prof. Baraka J. Maiseli alieleza maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo kukamilika kwa Jengo la HEET katika Kampasi ya Kijitonyama, maendeleo ya Kampasi ya Kagera, ujenzi wa kituo cha seva za kisasa (Advanced Server), usimikaji wa mtandao wa Wi-Fi chuoni, pamoja na maboresho ya miundombinu mingine inayolenga kuboresha mazingira ya kufundishia, kujifunzia na kufanyia kazi.

Pamoja na mafanikio hayo, kikao kilijadili changamoto mbalimbali zinazohitaji hatua za kimkakati, ikiwemo uwiano wa wahadhiri na wanafunzi, matumizi yasiyozingatia maadili ya teknolojia ya Akili Bandia (Artificial Intelligence – AI) katika shughuli za kitaaluma, uhitaji wa kuendelea kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, pamoja na kuimarisha mazingira ya kazi kwa watumishi.

Akihitimisha kikao hicho, Prof. Baraka J. Maiseli aliwahimiza watumishi kuendelea kushirikiana, kufanya kazi kwa weledi, ubunifu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao.

Alisisitiza kuwa mafanikio ya CoICT yanategemea mshikamano wa watumishi wote katika kufanikisha malengo ya kimkakati ya Ndaki na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ujumla.

Kikao hicho kilihitimishwa kwa mijadala na maoni kutoka kwa watumishi kuhusu namna ya kuendelea kuboresha utendaji kazi, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, na kuifanya CoICT kuwa kitovu kinachoongoza katika elimu, utafiti, ubunifu na teknolojia kwa maendeleo endelevu na shirikishi.